12 Juni 2024 - 15:47
Ripoti: Ukatili dhidi ya watoto katika maeneo ya vita uliongezeka sana 2023

Vitendo vya ukatili dhidi ya watoto viliripotiwa kuongezeka sana mwaka jana (2023) katika maeneo yanayoshuhudia vita na mapigano.

Hayo yamo katika ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inayoeleza ukatili dhidi ya watoto katika maeneo yaliokumbwa na migogoro kwa mwaka 2023. Ripoti hiyo inabainisha juu ya kuongezeka sana ukatili dhidi ya watoto kuanzia Palestina kufuatia mashambulio ya Israel dhidi ya Gaza hadi Sudan, Myanmar na Ukraine.

Ripoti ya kila mwaka ya Watoto walio katika Migogoro ya Kivita, inaonesha kuwa, kuna ongezeko kubwa la asilimia 21 la vurugu zenye kusababisha madhila ya watoto wa chini ya umri wa miaka 18, ikitolea mfano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burkina Faso, Somalia na Syria.

Kwa mara ya kwanza, ripoti hiyo imeliweka jeshi la utawala wa Kiizayuni wa  Israel kwenye orodha mbaya ya nchi zinazokiuka haki za watoto kwa mauaji na kulemaza watoto na kushambulia shule na hospitali.Sudan, ambako kumekuwa na vita kati ya majenerali wapinzani wanaowania mamlaka inayoendelea tangu 2023, kumeshuhudiwa ongezeko kubwa la asilimia 480 la hali ya ukiukwaji mbaya dhidi ya watoto. Katika ripoti hiyo mpya, Umoja wa Mataifa umeyataja mataifa kama Afghanistan, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika Kati, Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasiia ya Congo, Iraq, Mali, Msumbiji, Nigeria, Ufilipino, Somalia, Sudan Kusini, Syria, Ukraine na Yemen kama maeneo ambayo usalama watoto umeendelea kudidimia zaidi.

342/